Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA) unatarajia kusambaza majiko ya gesi ya kilo sita 19,530 kwa bei ya ruzuku (Nusu bei) katika Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 02 Disemba 2024 katika Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, kila Wilaya itapokea mitungi 3,255 ambayo itauzwa kwa shilingi elfu 20 badala ya shilingi elfu 40, huku nusu nyingine ya gharama ikigharamiwa na serikali kupitia ruzuku.
Akizungumza wakati wa kutambulisha mradi Mhandisi Mwandamizi wa Wakala wa nishati Vijijini (REA), Deusdedith Malulu amesema Serikali itagharamia shilingi bilioni 8.6 ikiwa na azma ya kufikia malengo ya Serikali ya matumizi ya 80% ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Aidha Mhandisi Malulu amesema mradi mwingine utakaogharamiwa na Serikali ni mradi wa usambazaji wa nishati ya umeme wa jua (Solar) ambapo nishati hiyo itauzwa kwa bei ya ruzuku ya 75% ambapo wanufaika ni wananchi waishio Visiwani na watapata nishati hiyo kwa shilingi laki moja hadi mbili badala ya makadirio ya shilingi laki 6.
"Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kufikisha nishati ya umeme katika maeneo yote nchini na kwa kutambua hilo imeona adha wanayoipata wananchi wa Visiwani na kuamua kuwaletea nishati ya umeme wa jua ambazo watazipata kwa punguzo la 75%".
Kadhalika mradi wa tatu ambao umetambulishwa ni mradi wa utoaji wa mikopo yenye masharti na riba nafuu iliyolenga kuwawezesha wananchi kujenga vituo vidogo vidogo vya mafuta maeneo y vijijini ili kurahisisha huduma ya upatikanaji wa mafuta maeneo ya vijijni.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya miradi hiyo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Mhandisi Chagu Nghoma ameishukuru REA na serikali kwa ujumla kwa kutoa ruzuku katika nishati hizo muhimu (Umeme wa Jua, majiko ya gesi pamoja na mikopo nafuu ujenzi wa Vitu vya mafuta vijijini) na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo adhimu.
Na Mwandishi wetu Mwanza