WAKAZI wa Kijiji cha Ngomai Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wamefanya harambee ya kumpongeza muuguzi wa kijiji hicho, Peter Mwakalosi kwa kufanya kazi kwa moyo wa ukarimu, upendo, kujitoa na kuzingatia maadili ya taaluma yake.
Harambee hiyo ilifanyika juzi kijijini hapo ambapo wananchi hao wamechanga zaidi ya Sh milioni nne kwa ajili ya kumnunulia kiwanja muuguzi huyo ili aweze kujenga na kuishi kijijini hapo hata atakapostaafu kazi.
Aidha katika risala wananchi wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na watumishi wenye kujitoa katika jamii akiwemo muuguzi huyo ambaye amekuwa mstari wa mbele kusaidia watu wa kijiji hicho na vijiji jirani.
Naye mgeni rasmi katika harambee hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kongwa, Dk Omary Nkullo amewapongeza wananchi wa Ngomai kwa kuandaa harambee hiyo, wameonesha moyo wa shukurani na jambo la kuigwa kwa watu wengine na kuongeza kuwa hilo ni deni ambalo anatakiwa kulipa muuguzi huyo.
Diwani wa Kata ya Ngomai, Mfaume Mlimila amemuomba mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kongwa asimhamishe muuguzi huyo kijijini hapo kwani anafanya kazi kubwa ya kutoa huduma nzuri ya afya na wananchi wanamkubali.
Mlimila alisema muuguzi huyo alipofika kijijini hapo mwaka 2005 amefanikiwa kuondoa dhana potofu ya wananchi kutibiwa kwa waganga wa kienyeji magonjwa ambayo awali hawakuamini kama yanaweza kutibiwa hospitalini na kupona.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dk Thomas Mchomvu alisema kuwa Kijiji cha Ngomai kimekuwa na sifa nzuri ndani ya wilaya . Alisema takwimu za mwezi zinaonesha wilaya huzalisha watoto 1,300 hadi 1,400 ambao kati yao, watoto 30 hadi 40 huzaliwa katika Zahanati ya Kijiji cha Ngomai huku kazi kubwa ikifanywa na muuguzi wao.