TANZANIA HATUNA MAAMUBUKIZI YA MPOX

KADUSHI MEDIA
By -
0

 

Serikali ya Tanzania imesema kuwa hakuna maambukizi ya ugonjwa wa Mpox nchini humo.

Hata hivyo, Mganga Mkuu nchini humo Profesa Tumaini Nagu amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kufuatilia kwa karibu ugonjwa wa Mpox na kuchukua hatua stahiki kuzuia ugonjwa huu kuingia nchini humo.

"Mpaka sasa, hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitika kuwa na maambukizi ya Mpox na nchi yetu ni salama. Hata hivyo, tunahitaji kuendelea kuchukua tahadhari kujikinga na ugonjwa huu," ilisomeka taarifa ya Profesa Nagu, kama ilivyochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa Wizara ya Afya ya Tanzania.

Katika taarifa yake, Mganga Mkuu katika serikali ya Tanzania ameuasa umma kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo kama vile kuepuka kugusana, kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana na kumbusu mtu mwenye dalili za Mpox, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono mara kwa mara na kuepuka kula au kugusa mizoga au wanyama mfano nyani au swala wa msituni.

Pia imewataka watu kuvaa barakoa iwapo itabidi kukaa na kuongea kwa karibu na mtu mwenye dalili za Mpox na kama ikibidi, kuwahi katika vituo vya huduma za afya wanapoona dalili za ugonjwa wa Mpox.


"Vile vile, tumeimarisha vituo vya huduma, maabara na upatikanaji wa dawa, vifaa kinga na tiba ili kutoa huduma stahiki endapo utaingia nchini," amesema.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa wa Mpox umeendelea kutolewa taarifa kutoka nchi mbalimbali duniani, ambapo hadi kufikia Juni 2024, jumla ya wagonjwa 99, 176 na vifo 208 vimethibitishwa.


Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)