Kamishna wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi (CP) Shabani Hiki amebainisha kuwa Serikali imedhamiria kuboresha mifumo ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi hasa mifumo ya Tehama.
Kamishna Hiki ameyasema hayo Agosti 05, 2024 Mkoani Mwanza wakati akizungumza na Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali katika uwanja wa Polisi Mabatini ikiwa ni ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Kanda ya ziwa.
Akiwa ameambatana na timu ya wataalamu wa masuala ya uchunguzi wa kisayansi ambao wamewasilisha mada mbalimbali za utekelezaji wa rasimu ya pili ya maboresho ya Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Hiki amesema Serikali imeamua kuboresha huduma ya Tehama kwa kuleta mawasiliano mazuri baina ya Jeshi la Polisi na Taasisi nyingine za Serikali ili kutoa huduma bora kwa wateja
Naye, Naibu Kamishna wa Polisi kutoka Kamisheni hiyo ya uchunguzi wa kisayansi (DCP) Mwamini amewataka wakuu wa upelelezi kutumia maabara ya kisasa ya uchunguzi wa kisayansi iliyopo Makao Makuu ndogo ya Polisi Dar es salaam ili ushahidi unaokusanywa na wapelelezi uwe na tija na kuthibitisha kosa mahakamani.
Kwa upande wake, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) John Mayunga amesisitiza kuendelea utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki jinai na kuimarisha huduma za kipolisi kwa kufuata Sheria, kuongeza matumizi ya Tehama, kuwajengea uwezo askari, kuboresha masuala ya kiutumishi na kuboresha miundombinu, zana na vifaa vya kazi.
Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa amesema wameendelea kusimamia nidhamu kwa Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali na kuchukua hatua za kinidhamu kwa wenye mienendo mibovu ndani ya Jeshi la Polisi ili kuwa na Jeshi lenye weledi wa kulinda raia na mali zao.