Katika kupambana na kuzuia ukatili wa kijinsia na watoto Mkoa wa Lindi, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wadau wa Taasisi mbalimbali za Kiserikali toka wilaya zote za mkoa wa Lindi wameweza kufanya kikao kazi katika ukumbi wa DDC Manispaa ya Lindi kilichodhaminiwa na Shirika la "ASUTA" kupitia "FHI360" na kuongozwa na Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Joyce Kitesho akiwa na mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Lindi Sagini Meja wa Polisi Siwabu Mikidadi.
Aidha Mkaguzi Kitesho amesema sababu kubwa za ukatili wa kijinsia na watoto ni umasikini, imani potofu, ukosefu wa elimu, mfumo dume, tamaa ya kupenda vitu vilivyo nje ya uwezo, kutoheshimiana kwa wanafamilia, mila na desturi potofu, kujiunga na makundi ya wahuni, tamaa ya mapenzi na kukata tamaa ya maisha. Kutokana na hayo amesema inabidi kila mmoja atimize wajibu wake kwa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto kwa kupambana na vyanzo hivyo.
Aidha, Sagini meja Siwabu amesema athari za ukatili wa kijinsia na watoto ni vifo, mimba za utotoni, kilema cha kudumu, kuharibika kisaikolojia, kufifisha malengo ya baadae kwa watoto, umasikini na kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa. Pia amewataka waliohudhuria kikao hicho kutoa ushirikiano Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu sambamba na taarifa za vitendo au viashiria vya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili wa watoto.
Pia kikao hicho kiliweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia na watoto ambayo itapimwa kila baada ya miezi mitatu.
Na mwandishi wetuLindi