Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi, DCP Wilbrod Mutafungwa ameongoza vyombo vya usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mkoa wa Mwanza kufanya matembezi ya hiari (route match) katika mitaa ya Jiji la Mwanza.
Matembezi hayo yaliyofanyika leo Jumamosi Agosti 17,2024, yamejumuisha askari kutoka Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji mkoani humo.
Mazoezi hayo ya pamoja yanalenga kuimarisha ushirikiano na utimamu wa mwili na akili katika kutekeleza majukumu ya kulinda nchini, raia na mali zao.
Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Kamanda Mutafungwa amesema mbali na kuongeza ari katika utekelezaji majukumu ya ulinzi na usalama, yanaongeza ushikiano baina yao huku akiwapongeza askari walioshiriki.
"Mazoezi haya yatatusaidia kufahamiana kwani hivi karibuni tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo watu wanategea usalama siku za kupiga kura, wakati wa kampeni na wakati wa kupeleka vifaa kwenye vituo vya kupigia kura,” amesema DCP Mutafungwa.
Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Magereza, Ramadhan Ngoi kwa niaba ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza amesema mazoezi ni muhimu kwa afya huku akitoa ushauri kwa askari kushiriki kikamilifu.
Naye, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto Wilaya ya Ilemela mkoani humo, Deus Ruta ameshauri mazoezi hayo yawe endelevu miongoni mwa askari wa majeshi hayo.
Pia kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Uhamiaji mkoa wa Mwanza (SACI) Colla Kayumba amesema kulingana na majukumu yanayofanywa na vyombo hivi ni muhimu sana kufahamiana na kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu.
Hata hivyo mazoezi haya yameambatana na michezo mbalimbali ikiwemo kuvuta kamba, kukimbiza kuku na kutembea na kijiko kilichowekwa yai mdomoni.