Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na wananchi wa kisiwa cha Yozu na Burihaeke wilaya ya Sengerema wameendelea na utafutaji wa watu watano ambao hadi sasa hawajaonekana walipo baada ya mtumbwi wao waliokuwa wakisafiria kuzama maji na wenzao 17 kufanikiwa kuokolewa huku mmoja akipatikana akiwa amefariki.
Tukio hilo lilitokea Agosti 05,2024 majira ya 2:00 usiku katikati ya kisiwa cha Yozu na Ziragula wakati wakitokea kwenye sherehe ya mashabiki wa Yanga (Yanga day) iliyofanyika kisiwani Yozu wakielekea kitongoji cha Itabagumba baada ya mtumbwi wao kuingia maji na kuzama.
Akizungumza na wananchi wa kisiwa hicho baada ya kukagua eneo la tukio, kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Naibu kamishina wa Polisi (DCP) Wilbord Mtafungwa amewataka mmiliki wa mtumbwi uliopata ajali aitwaye Sebastian Balakoa na nahodha wa mtumbwi huo aliyefahamika kwa jina moja la Otieno kujisalimisha kwa Jeshi la Polisi ili waweze kuhojiwa kuhusiana na ajali hiyo kwani walitoweka baada ya ajali hiyo.
Aidha, kamanda Mutafungwa amewataka wananchi hususani wavuvi kushirikiana na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama katika kuwatafuta watu wengine watano ambao hawajapatikana. Pia, amewapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa jitihada kubwa walizoonesha na kufanikiwa kuwaokoa watu 17 wakiwa hai baada ya ajali hiyo kutokea.
Pia, amekumbusha mamlaka zinazohusika na usalama majini kukagua mtumbwi ili kujiridhisha na uimara wake pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuzingatia umuhimu wa kuvaa maboya (life Jacket) wawapo katika usafiri wa majini na kuhakikisha kwamba mitumbwi yote ya ziwani inakuwa na vifaa vya kujiokoa endapo ajali ikitokea.
Sambamba na hayo, Kamanda Mutafungwa pomoja na mkuu wa kikosi cha wanamaji mkoa wa Mwanza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Wenceslaus Muchunguzi, wametumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa wavuvi na wananchi wengine juu ya umuhimu wa kuvaa Maboya pindi wawapo kwenye usafiri wa majini na kutopanda mitumbwi ambayo tayari imezidisha abiria kupita uwezo wake hivyo inasababisha kuhatarisha usalama wa maisha yao.
Na Pascal Kadushi