Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameiambia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuwa Mkoa wa Mwanza haujawahi kukwamisha shughuli au jambo lolote ambalo serikali imelipanga, kwa maanaa hiyo pia hata uchaguzi Mkoani humo utakuwa wa amani na utulivu.
Mhe. Mtanda ameyasema hayo mapema leo Agosti 09, 2024 wakati alipokuwa akiipokea na kuikaribisha Mkoani Mwanza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliyowasili Mkoani hapo kwa ajili ya mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amesema serikali ya Mkoa tayari imeshaanza kuifanya kazi hiyo kwa kutoa elimu ya uchaguzi na upigaji kura kwa wananchi kupitia mikutano mbalimbali ambayo imekuwa ikifanyika Mkoani humo na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo mbalimbali vitakavyoainishwa ili warekebishe na kuandika taarifa zao.
"Tumejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, na kuanzia sasa niseme tu ofisi yangu itatoa ushirikiano wa kutosha mpaka pale uchaguzi utakapokamilika".
Naye Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele amesema wamedhamiria kufanya maandalizi ya kutosha kuelekea uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura na kwa Mkoa wa Mwanza wameanza na mkutano huo utakaowashirikisha wadau wa uchaguzi ambao ni vyama vya siasa, dini, asasi na makundi mbalimbali.
"Tume imeendelea na maandalizi mbalimbali ikiwemo ya kutoa elimu ya upigaji kura kupitia vyombo mbalimbali vya habari, mikutano ya hadhara, pamoja na kutumia magari ya matangangazo". Amesema Mhe. Jaji Mwambelege.
Aidha Mwenyekiti wa Tume hiyo pia amemtaka Mkuu wa Mkoa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha elimu inasambaa zaidi kwa wadau wote kwa kuwa ana wasaidizi wengi hususani katika maeneo ya ngazi za chini za utawala.
Uboreshaji wa daftari la mpiga kura kwa Mkoa wa Mwanza unatarajiwa kuanza rasmi kuanzia 21 - 28 mwezi Agosti 2024.