Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza Mwl. Martin Nkwabi amewataka Maafisa Takwimu wa Halmashauri za Mkoa wa Mwanza kuhalalisha uwepo wao kwa kufanya kazi kwa bidii na kuboresha utendaji kazi wao ili kuifanya kazi ya kitengo hicho kuonekana.
Mwalimu Nkwambi ametoa wito huo leo Agosti 15, 2024 wakati alipokuwa akifungua kikao cha Maafisa Vifaa na Takwimu Msingi na Sekondari kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mwl. Nkwabi amesema kwa kipindi cha hapo nyuma kumekuwa na vitengo mbalimbali ndani ya Idara ya Elimu lakini kutokana na kutofanya vizuri kwa vitengo hivyo vimefutwa hivyo amewataka Maafisa hao pia kubadilika na kuhalilisha uwepo wao.
"Sisi tunatakiwa kubadilisha utendaji kazi wetu, Katika miaka kama 20 hivi vitengo katika Idara ya Elimu zimekuwa zikibadilika badilika kwa sababu wale waliopewa majukimu hayo walishindwa kuhalalisha zile nafasi zilizokuwepo na mimi sitaki yawakute hayo". Amesema.
Takwimu za elimu ni nyingi sana ndio maana mkawekwa nyinyi kuna takwimu za vitabu, kuna idadi ya Wanafunzi wenye ulemavu, Afisa Michezo anahitaji takwimu za Wanafunzi wanaoweza kucheza michezo mbalimbali, mkifanya vizuri katika uratibu wa sekta yenu hamtoamini mtakuwa mnatafutwa sana huko kwenye Halmashauri zenu kwa sababu kila mtu atahitaji kupata takwimu sahihi kutoka kwenu. Ameongeza Afisa Elimu.
Sambamba na hayo Afisa Elimu huyo amewataka Maafisa hao kuhuisha takwimu zao mara kwa mara kwa sababu mambo hubadilika, takwimu za mwaka jana sio za mwaka huu mambo mengi hapa kati yanatokea ikiwemo uhamisho wa Waalimu na Wanafunzi, Walimu wanaokwenda kusoma.
Aidha Afisa Elimu huyo amewataka Maafisa hao kufanya kazi kwa ushirikiano na Maafisa wengine kutoka Idara za Elimu kwani wote ni watumishi wa elimu na ikitokea unahitajika msaada wowote katika Idara basi mtu yoyote aweze kufanya shughuli hiyo.
Na mwandishi wetu Mwanza