Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Mei 9, 2024 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa amekutana kwa nyakati tofauti na Wakuu wa Taasisi za Umma, viongozi wa Wamachinga na viongozi wa Wafanyabiashara kwa lengo la kufahamiana na kufahamu shughuli zao.
Akianza mkutano huo na Wakuu wa Taasisi za Umma, Mkuu huyo wa Mkoa amewakumbusha kutambua wajibu wao kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati.
"Rais Samia ameonesha kwa vitendo anavyopigania maendeleo y wananchi,na sisi tunavyotoa huduma bora wananchi watazidi kuifurahia Serikali yao" Mkuu wa Mkoa.
Amewataka viongozi hao kutekeleza wajibu wao kwa kuimarisha nidhamu ya utumishi wa umma kwa kufanya kazi kwa upendo, kuheshimiana na kuepuka aina yoyote ya unyanyasaji au kupokea rushwa kutoka kwa wananchi.
Amesema yupo mbioni kuanza ziara kutembelea maeneo yote mkoani humo ili kujionea maendeleo ya wananchi na changamoto zinazowakabili.
"Ndugu viongozi mkutano huu sio wa kusikiliza changamoto zenu na kuzitolea majibu hapa la hasha! lengo ni kufahamiana na kujua shughuli zenu mkitambua sina muda mrefu tangu nihamishiwe hapa nikitokea Mara". Amesema Mhe. Mtanda.
Katika mkutano wake wa pili na viongozi wa Wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga, Mhe.Mtanda amewaahidi kuwatembelea maeneo yao na kujionea hali halisi kabla ya kuchukua maamuzi yenye malengo ya kuboresha shughuli zao.
"Mkoa wa Mwanza una jumla ya masoko 50 yenye wafanyabiashara wadogo 19,969 ambao wapo katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza. Amesema Yesaya Sikindeni, Afisa Biashara Mkoa.
"Nimesikia changamoto zenu uzuri nina uzoefu wa kutosha na kero zinazo wasumbua, nimesikia taarifa fupi kutoka kwa Afisa biashara ikiwemo hali ya masoko na mazingira yenu, kuweni na utulivu na fanyeni shughuli zenu kwa kuheshimu maelekezo mliyopewa na Serikali." Mkuu wa Mkoa.
Akimalizia mkutano huo na viongozi wa Wafanyabiashara wakubwa, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha anatambua mchango wao katika pato la Taifa na kusisitiza kuendelea kushirikiana katika ujenzi wa Taifa.
BAADHI YA PICHA ZA MATUKIO