Wakati taratibu za mazishi ya Rais wa Iran, Ebrahim Raisi zikiendelea, Makamu wa Rais Mohammad Mokhber anayetarajiwa kurithi nafasi hiyo kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, ameongoza mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri.
Raisi amefariki kwenye ajali ya helikopta jana Mei 19, 2024 akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Hossein Amir-Abdollahian ambaye pia amefariki dunia wakati walipokuwa wakirejea kutoka nchi jirani ya Azerbaijan kwenye hafla ya uzinduzi wa bwawa.
Ajali hiyo imetokea eneo la milimani katika jimbo la East Azerbaijan, ambapo pia ndani ya helkopta walikuwa pamoja na Gavana wa Mkoa wa Azerbaijan Mashariki, Malek Rahmati wa Iran na mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Mkoa wa Azerbaijan Mashariki, Ayatollah Mohammad Ali Ale-Hashem pamoja na walinzi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Iran, iwapo Rais atafariki akiwa madarakani, kifungu cha 131 kinasema makamu wa kwanza wa Rais ndiye atakayeshika madaraka, huku baraza linalojumuisha makamu wa kwanza wa rais, spika wa bunge na mkuu wa mahakama lazima lipange uchaguzi wa Rais mpya ndani ya muda usiozidi siku 50.
Makamu wa Rais Mohammad Mokhber anatarajiwa kuwa rais wa mpito wa nchi hiyo, ambaye atasaidia kuandaa uchaguzi wa rais ambao unapaswa kufanyika ndani ya siku 50 baada ya kifo cha rais.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Mokhber aliyezaliwa Septemba 1, 1955, anaonekana kuwa karibu na Kiongozi Mkuu Ali Khamenei, ambaye ana kauli ya mwisho katika masuala yote ya serikali. Mokhber alikua makamu wa kwanza wa rais mwaka 2021 wakati Raisi alipochaguliwa kuwa rais.
Mokhber alikuwa sehemu ya timu ya maofisa wa Iran ambao walitembelea Moscow Oktoba, 2023 na walikubaliana kusambaza makombora ya ardhini hadi ardhini na droni zaidi kwa jeshi la Russia.
Timu hiyo pia ilijumuisha maofisa wawili wakuu kutoka Walinzi wa Mapinduzi ya Iran na ofisa kutoka Baraza Kuu la Usalama wa Taifa.
Mokhber hapo awali alikuwa mkuu wa mfuko wa uwekezaji unaohusishwa na kiongozi mkuu (Setad).
Mnamo mwaka 2010, Umoja wa Ulaya ulimjumuisha Mokhber kwenye orodha ya watu na mashirika yanayowekewa vikwazo kwa madai ya kuhusika katika "shughuli za nyuklia au za makombora ya ballistic". Miaka miwili baadaye, walimwondoa kwenye orodha hiyo.
Mnamo mwaka 2013, Idara ya Hazina ya Marekani iliongeza Setad na kampuni 37 ambazo ilizisimamia kwenye orodha ya mashirika yaliyowekewa vikwazo.
Setad, jina lake kamili ni Setad Ejraiye Farmane Hazrate Emam, au Makao Makuu ya Kutekeleza Amri ya Imamu, ilianzishwa chini ya amri iliyotolewa na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu, mtangulizi wa Khamenei, Ayatollah Ruhollah Khomeini.
Ilielekeza wasaidizi kuuza na kusimamia mali ambazo zinadaiwa kutelekezwa katika miaka ya machafuko baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 na kuelekeza sehemu kubwa ya mapato hayo kwa misaada.
Salamu za rambirambi
Baada ya kutokea msiba huo, viongozi na taasisi mbalimbali duniani wamekuwa wakitoa salamu za rambirambi. Miongoni mwao ni Kundi la Hamas ambalo limetoa taarifa ikimshukuru rais wa Iran Ebrahim Raisi na waziri wa Mambo ya nje Hossein Amir-Abdollahian kwa msaada wao katika vita vyake dhidi ya Israel baada ya vifo vyao jana.
“Viongozi hawa waliunga mkono mapambano halali ya watu wetu dhidi ya chombo cha Kizayuni, walitoa msaada wa thamani kwa upinzani wa Palestina, na walifanya jitihada zisizochoka katika mshikamano na msaada katika mabaraza na nyanja zote kwa watu wetu katika Ukanda wa Gaza unaosimama imara. Pia walifanya juhudi kubwa za kisiasa na kidiplomasia kusimamisha uchokozi wa Kizayuni dhidi ya watu wetu wa Palestina,” imesema taarifa ya Hamas.
Kwa upande mwingine, Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, alisema asubuhi hii kwamba "EU inaeleza rambirambi zake za dhati kwa kifo cha rais Ebrahim Raisi na waziri wa mambo ya nje Hossein Amir-Abdollahian, pamoja na wanachama wengine wa ujumbe wao na wafanyakazi katika ajali ya helikopta."
Ubalozi wa Russia huko Tehran pia umetuma rambirambi zake siku ya Jumatatu kufuatia kifo hicho, ikimlilia Raisi aliyeisambazia Urusi silaha kwa ajili ya matumizi katika uvamizi wake wa Ukraine.
“Fikra zetu ziwaendee familia,” aliongeza. Ubalozi wa Russia huko Tehran.
Kwa upande wake Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mohammed bin Zayed Al Nahyan, amesema nchi yake inasimama kwa mshikamano na Iran katika kile alichokiita "wakati mgumu," na kutoa rambirambi kwa serikali ya Iran na watu wa Iran.
Na Pascal Kadushi