Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa iwapo jamii itapunguza matumizi ya pombe isiyo zimuliwa yaliyokithiri itasaidia kukabiliana na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.
Waziri Ummy amesema hayo Aprili 23, 2024 Jijini Dar Es Salaam wakati akifungua na kuhutubia Mkutano unaojadili namna ya kukabiliana na Magonjwa Yasiyoambukiza Barani Afrika, ambapo amesema kiwango cha Matumizi ya pombe kali nchini kimongezeka kutoka Lita 9.1 mpaka Lita 10 .4 kwa Mwaka.
“Tanzania tunaona ongezeko la unyaji Mkubwa wa pimbe wakati tumepunguza watu wanaokunywa pombe, tulikuwa na watu wanaokunywa pombe mwaka 2019 ilikuwa ni kama 26% tumeipunguza mpaka asilimia 20, lakini kiwango cha Pombe kimeongezeka kutoka lita 9.1 kwa mwaka mpaka 10.4 kwa mwaka, tuepuke unywaji wa pombe uliokithiri”
Ameongeza kuwa Tanzania kama Nchii nyingine za Afrika inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza.
“Tunaona ongezeko kubwa la watu wenye magonjwa yasiyoambukiza hususani shinikizo la juu la damu, kisukari, Saratani lakini pia Selimundu kama nchi tutaendela kuwekeza katika mikakati ya kinga na kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu na huduma dhidi ya magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza” amesema Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy amesema Serikali inaendelea na kutoa Chanjo ya kukinga dhidi ya Saratani ya Mlango wa Kizazi.
“Tunaweza tukatokomeza Saratani ya Mlango wa Kizazi kama tutawapa watoto wetu chanjo ya dhidi ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya Kizazi (HPV) na inatolewa kwa mabinti ambao hawajaanza kujamiiana kwa sababu vile virusi vya HumanPapiloma vinatoka kwa mwanamke, kwahiyo tunaatoa kwa mabinti ya miaka 9 mpaka 14, tunaweza baada ya miaka 10 hadi 20 tukasahau kuhusu saratani ya Mlango wa Kizazi” amsema Waziri Ummy.
Na Pascal Kadushi